Skip to main content
x
Salamu za rambirambi kutokana na kifo cha aliyekuwa rais wa awamu ya tano wa jamhuri ya muungano wa tanzania

Salamu za rambirambi kutokana na kifo cha aliyekuwa rais wa awamu ya tano wa jamhuri ya muungano wa tanzania

Bodi ya Wakurugenzi, Wanachama, Menejimenti na Wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za Ardhi (HAKIARDHI) tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya majonzi ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi 2021.

Kwa sababu hiyo tunaungana na Watanzania wote katika maombolezo ya kifo cha mpendwa Rais Ndugu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kwa namna ya kipekee Taasisi ya HAKIARDHI inakumbuka na kuenzi mchango mkubwa wa Hayati Rais Dkt. John Magufuli katika kipindi chote cha uongozi wake katika utetezi wa haki za wazalishaji wadogo nchini kwenye sekta zote kama vile kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo, sekta isiyo rasmi, madini na sekta nyinginezo.

Kuna maamuzi mengi ambayo Hayati Rais Dkt. John Magufuli aliyafanya na ambayo yatadumu kwenye mioyo ya wazalishaji wadogo, maamuzi hayo ni pamoja na;

  • Kufuta hati za mashamba yote ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali nchini na kuagiza kuwa mashamba hayo yagawiwe kwa Wakulima na Wafugaji wenye uhitaji wa ardhi ya kilimo na ufugaji.
  • Kupinga vikali kitendo cha ugawaji wa ardhi kutoka kwenye mashamba yaliyofutiwa hati kwenda mikononi mwa watu wachache.
  • Kuunda Kamati ya Mawaziri ya kisekta kushughulikia migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji nchi nzima pamoja na kuridhia uamuzi wa kuvirudishia hadhi vijiji 920 kati ya 975 ambavo vilikuwa vifutwe kwa madai ya kuwa vipo ndani ya maeneo ya hifadhi.
  • Kuwataka Mawaziri kuondoa zuio la wakulima kufanya shughuli za kilimo pembezoni mwa mito hasa kipindi cha kiangazi ili kuweza kujipatia mazao ya kujikimu na kuagiza kama kuna haja basi sheria zifanyiwe mabadiliko kuruhusu jambo hilo.
  • Kusisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza katika usikilizwaji wa mashauri na uandishi wa nyaraka za mahakama kama vile hukumu ili kuwezesha wananchi kuelewa vyema haki na wajibu wao ulivyoainishwa kwenye hukumu zinazotolewa na mahakama.

Kwa mifano hii michache na mingine mingi iliyopo inadhihirisha namna ambavyo Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ataendelea kukumbukwa na kuishi kwenye mioyo ya wazalishaji wadogo kwa miaka mingi ijayo kutokana namna alivyojipambanua kuwa mtetezi na mlinzi wa maslahi yao popote pale nchini.
Roho ya Marehemu Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli ipumzike mahali pema peponi, Amina.

IMETOLEWA NA BODI YA WAKURUGENZI YA TAASISI YA HAKIARDHI LEO TAREHE 18 MACHI 2021, DAR ES SALAAM