Skip to main content
x
Frola Mgendwa

Wewe ni mwanamke siwezi kukupa ardhi

Simulizi ya mapambano ya haki za ardhi kwa wanawake kama ilivyosimuliwa na Frola Mgendwa wa Keiji cha Lugalo Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa

Nakumbuka ilikuwa mwaka 1994 nilikwenda kwa baba kuomba shamba, baba akasema hivii, shamba hanipi kwa sababu mimi ni mwanamke nitapata baadaye.

Nikakaa baada ya miaka mitano nikaenda tena kuomba ardhi akaniambia nilishakwambia wewe ni mwanamke siwezi kukupa ardhi. Nilichukua hatua ya kwenda kuomba ardhi kwa kaka, nilivyoenda kwa kaka, akasema nakuazimisha shamba ila sikupi umiliki. Nililima mpaka mwaka 2015 nilipopata mafunzo juu ya haki za ardhi kwa wanawake.

Nilipopata mafunzo niliona ni vyema nieneze ile elimu kijijini kwangu, nikaanza kuelimisha wenzangu katika vikundi, pia nikaenda nyumbani nikakusanya familia, nikamweleza baba siku ya kwanza juu ya umuhimu wa mtoto wa kike kumiliki ardhi, nikaenda tena siku ya pill akanielewa, alivyonielewa akatuita familia nzima tukaenda shambani akatugawia watoto wake watatu shamba lake la ekari saba ambapo kila mmoja alipata ekari mbili, ekari moja ikabaki kwa matumizi ya pamoja.

Hill ni jambo ambalo najivunia mno, ikumbukwe kwa mila zetu sisi Wahehe sio rahisi kwa mwanamke kumilikishwa ardhi au mali yoyote ya kudumu, tunaamini tutapata mali katika ndoa zetu. Na mara nyingi tunapata changamoto kubwa sana ikitokea tumeachika au waume zetu wakifariki. Kitu kigumu zaidi ni kuwa kimbelembele katika kutetea haki za wanawake, jamii inakuona mwanamke asiye na nidhamu. Ila kiukweli kwa sasa jamii katika kijiji chetu tumeelimika vya kutosha na mwanga unaonekana.