Skip to main content
x
Taasisi ya HAKIARDHI imefanya uchambuzi wa bajeti ya Wizara ya ardhi

Taasisi ya HAKIARDHI imefanya uchambuzi wa bajeti ya Wizara ya ardhi

Taasisi ya HAKIARDHI imefanya uchambuzi wa bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2020/21 ili kubaini ni kwa kiasi gani bajeti hiyo inakidhi mahitaji ya wazalishaji wadogo hususani wanawake katika upatikanaji wa ardhi, matumizi, umiliki na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

 

Uchambuzi wa bajeti uliainisha masuala kadhaa ya msingi mojawapo ikiwa kuhakikisha kuwa ardhi inajumuishwa katika sekta kipaumbele ili kupata bajeti ya kutosha kutatua changamoto zilizopo katika sekta hususani utatuzi wa migogoro ya ardhi na upangaji wa matumizi ya ardhi.

 

Vilevile uanzishwaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ni eneo lililogusiwa katika uchambuzi huu kutokana na uchache wa mabaraza haya lakini umuhimu wake ukiwa ni mkubwa sana katika kusuluhisha kesi za masuala ya ardhi nchini.

 

Upanukaji wa miji na kukua kwa vijiji ni suala jingine lililojadiliwa kwa kina katika uchambuzi huu kwa kuainisha kuwa, pamoja na umuhimu wa kukua kwa miji lakini kuna ulazima wa kulinda ardhi za vijiji kwakuwa huko ndiko wazalishaji wengi wadogo wanapozalisha mali na rasilimali kubwa ikiwa ni ardhi.

 

Pichani ni washiriki wa kikao kilichofanyika tarehe 12/02/2021 Jijini Dodoma ambapo wawakilishi wa Wizara mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tume ya mipango ya  Matumizi ya Ardhi nchini na wadau kutoka asasi kumi na moja zinazotekeleza mradi wa haki za ardhi kwa wanawake ambazo ni CEDESOTA, UMWEMA, COSITA, UCRT, WODSTA, TAWLA, AVCD, TARWOC, MPLC na ICISO walishiriki.Mradi huu unafadhiliwa na Foundation for Civil Society.