Mradi wa Ardhi Yetu
Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za Ardhi (LARRRI/HAKIARDHI) ni Taasisi ya Kiraia iliyoanzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kufanya Utafiti na Utetezi wa haki za ardhi kwa Wazalishaji Wadogo wadogo nchini ili kukuza uelewa wao katika Sera na Sheria za ardhi na kuimarisha mifumo ya usimamizi, matumizi na utatuzi wa migogoro ya ardhi. HAKIARDHI ilisajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni Sura ya 212 mwaka 1994 na kisha mwaka 2019 usajili ulihamishwa chini ya Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa usajili namba 00NGO/R2/00012.
10 Februari 2021 Taasisi ya HAKIARDHI iliingia makubaliano ya ufadhili na Shirika la Care International Tanzania kutekeleza Mradi wa Ardhi Yetu Programme II kwa kiasi cha fedha za kitanzania Shilingi Milioni 191,413,092 kwa kipindi cha kuanzia Januari 2021 hadi Oktoba 2021 katika wilaya za Kilombero, Morogoro vijijini, Kilolo na Mufindi.
Lengo la Mradi huu ni kutoa elimu kuhusu haki za ardhi na mabadiliko ya tabia nchi kwa lengo la kuboresha mfumo wa umiliki wa ardhi na kuongeza ustahimilivu kwa wazalishaji wadogo hasa Wanawake kwenye kilimo na ufugaji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.