Skip to main content
x
Maadhimisho ya dunia ya siku ya wanawake waishio vijijini mwaka 2021

Maadhimisho ya dunia ya siku ya wanawake waishio vijijini mwaka 2021

“Wanawake wa Vijijini katika uzalishaji wa Chakula kwa wote”.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake Vijijini ilianzishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Azimio lake la namba 62/136, tarehe 18 Disemba 2007. Lengo la kuazimisha siku hii kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ni kutambua na kuenzi "majukumu muhimu na mchango wa wanawake waishio vijijini katika kusukuma gurudumu la maendeleo vijijini, kukuza sekta ya kilimo vijijini, kuboresha uhakika na usalama wa chakula na kutokomeza umaskini vijijini.” Siku hii huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 15 ya mwezi Oktoba.
Kauli mbiu ya siku hii kwa mwaka 2021 inaangazia katika “wanawake wa vijijini katika uzalishaji wa chakula kwa wote” katika lugha ya kiingereza dhima ya siku hii imewekwa kama ifuatavyo “Rural Women Cultivating Good Food for All”.

Wanawake wa vijijini wamekuwa na majukumu makubwa katika kuendeleza kaya wanazoishi na jamii kwa ujumla hususani katika maeneo ya vijijini, kwa miaka mingi nafasi ya mwanamke wa kijijini imekuwa haionekani kuwa ya tija na inayozungumzwa na kuandikwa sana kama ambavyo makundi mengine ya kijamii yanavyopewa kipaumbele. Ni dhahiri kuwa wanawake ndio walio wengi katika sekta ya kilimo kuliko wanaume ingawa katika taswira ya haraka haraka wanaume wamekuwa wakitajwa zaidi kuwa wenye nguvu na misuli ya kujiingiza katika kilimo. Sio tu katika kilimo, wanawake wa vijijini wapo mbele katika sekta isiyo rasmi kwa kujihusisha na biashara ndogo ndogo mbalimbali kwa lengo la kuingiza kipato ndani ya familia. Wanawake hawa hawa ndio wanaojihusisha na utoaji huduma mbalimbali katika ngazi ya familia na jamii wakati mwingine pasipo malipo yoyote.
Katika hali halisi, wanawake vijijini wanaishi katika umaskini kutokana na upatikanaji duni na hafifu wa huduma mbalimbali za kijamii kama vile afya, maji, makazi bora, elimu, miundombinu na mawasiliano dhabiti, n.k. Kidunia takwimu zinaonesha kuwa umasikini uliokithiri unapungua ulimwenguni pote lakini bado kuna watu wapatao bilioni 1 ulimwenguni pote ambao wanaendelea kuishi katika mazingira ya umasikini hususani katika maeneo ya vijijini, tafiti zinaonesha kuwa viwango vya umasikini ni vikubwa zaidi katika maeneo ya vijijini kuliko mijini. Katika kukabiliana na umasikini kwenye maeneo ya vijijini kilimo na ufugaji ndio shughuli kubwa zinazofanywa, takwimu zinaonesha kuwa katika bara la Asia na Kusini mwa Jangwa la Sahara kilimo kinazalisha asilimia 80 ya chakula chote, vile vile kilimo kinaendesha maisha ya watu wapatao bilioni 2.5.

Katika bara la Afrika changamoto kubwa katika kilimo hususani kwa wazalishaji wadogo ambao miongoni mwao ni wanawake ni uhaba wa ardhi inayotosheleza, ukosefu wa mikopo rafiki inayoendana na maisha na uchumi wa wazalishaji wadogo, ukosefu na uhaba wa pembejeo za kilimo, soko lisilokuwa la uhakika la masoko ya mazao yanayozalishwa kila msimu, uwepo wa madalali unaopelekea wakulima kupata kipato duni kutokana na kulanguliwa mazao yao.

Wanawake kwa ujumla ni waathirika wa ubaguzi unaotokana na mila na desturi, muundo wa kiuongozi na mitazamo ya kijamii katika mgawanyo wa majukumu kwa mwanaume na mwanamke. Ingawa kwa kiasi kikubwa wanawake wa vijijini ndio wanaoathirika zaidi kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi na kwa wakati kutokana na uduni wa miundombinu katika maeneo ya vijijini. Vile vile, mashirika na taasisi zilizo nyingi za kiserikali, kiraia na kibinafsi zimekuwa hazipeleki miradi mingi ya elimu na mafunzo mbalimbali kwenye maeneo ya vijijini ukilinganisha na upendeleo mkubwa uliopo kwenye maeneo ya mijini.

Hata katika masuala ya uongozi kitakwimu wanawake wa waishio vijijini ni wachache kwenye nafasi za uongozi kwenye ngazi za vitongoji, vijiji na kata ukilinganisha na wanawake waliopo mijini. Katika mgawanyo wa rasilimali na mali bado wanawake wa vijijini wanakabiliana na changamoto ya kupata haki iwapasayo ukilinganisha na mchango wao na nguvu kubwa wanayoiweka katika kuzitafuta na kuzitunza mali na rasilimali husika. Kwa mfano, katika maeneo ya vijijini ambazo HAKIARDHI inatekeleza miradi kama vile Kilolo, Mufindi, Kilindi, Morogoro, Mkuranga, Kilombero, Kilosa, n.k, wanawake walio wengi ndio wanaojishughulisha na kilimo kwenye ardhi ambazo wao hawana umiliki wa moja kwa moja. Ndio maana inapotokea ndoa imevunjika wanawake ndio wamekuwa wakipoteza ardhi kwa sababu kwa kipindi chote cha maisha ya ndoa yake alikuwa akilima kwenye mashamba ya mume wake. Hata katika familia walizozaliwa wasichana wamekuwa aidha hawapati kabisa urithi wa ardhi au wanapata ardhi ndogo sana kutoka kwa wazazi wao, pamoja na ukweli kuwa watoto wa kike ndio wanaokwenda shambani kulima na Mama zao toka wakiwa wadogo wakati kaka zao wakiwa mashuleni au nyumbani.

Mwaka huu dunia inapoadhimisha siku ya wanawake waishio vijijini ikiwa na kauli mbiu ya wanawake wa vijijini katika uzalishaji wa chakula kwa wote ni muhimu kuibua na kujadili matatizo yanayowakabili wanawake waishio vijijini kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo haya. Wanawake wa vijijini hawana uhakika wa kumiliki ardhi hususani katika kipindi hiki ambacho kuna wimbi la uuzaji wa ardhi na ugawaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji. Ni muhimu sana kuweka mikakati ya kuilinda ardhi ya vijiji ili iendelee kuwa kwenye matumizi na umiliki wa wanavijiji wenyewe hususani wanawake.

Vile vile, athari za mabadiliko ya tabia nchi zimeathiri shughuli za kilimo kwenye maeneo ya vijijini hadi wakati mwingine kupelekea uhaba wa chakula. Serikali na wadau wengine waongeze jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu na kwa kuwashirikisha wanavijiji hasa wanawake ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wake unakuwa shirikishi. Vile vile, ujuzi wa asili kutoka kwa wanavijiji wenyewe upewe kipaumbele katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ujuzi wao wa asili usipuuzwe katika kutunga sera, kuanzisha na kutekeleza miradi na kufanya maamuzi.
Uhakika wa pembejeo za kilimo ikiwa ni pamoja na mbolea, mbegu na madawa yapatikane kwa wakati kwenye vijiji vyote na kwa bei ambayo sio kandamizi ili kuwawezesha wanawake walio katika kilimo kukifanya kilimo kwa unafuu na urahisi zaidi. Wakulima wadogo wadogo vijijini wamekuwa na malalamiko ya urasimu katika kupata pembejeo za kilimo, hata pale inapobidi wapate pembejeo hizi kwa mikopo, mikopo hiyo sio rafiki kwa sababu huwa na riba kubwa na pindi mkulima anaposhindwa kulipa kwa wakati hupoteza mazao yake aliyoyahangaikia kwa msimu mzima.

Kukosekana kwa soko madhubuti na imara la mazao yanayozalishwa vijijini kumeathiri wakulima wadogo wadogo ambao ni pamoja na wanawake. Wakulima wadogo hutumia muda mrefu na mtaji duni katika kulima mazao bora sana kwahiyo wanapokumbana na changamoto ya ukosefu wa masoko inakuwa kikwazo kikubwa kwao katika kuendeleza kilimo chenye tija. Ukosefu wa masoko ya uhakika kumepelekea uwepo wa madalali ambao huwalangua wakulima mazao yao kwa bei ya chini wakati wao wakipata faida kubwa wanapopeleka katika masoko ya mijini na nje ya nchi.

Kukithiri kwa migogoro ya ardhi ya aina tofauti tofauti kama vile migogoro baina ya wakulima na wafugaji, mamlaka za hifadhi za wanyamapori na wanavijiji, migogoro ya ardhi ya mipaka baina ya vijiji na migogoro inayohusisha wawekezaji na wanavijiji. Migogoro hii kwa kiasi kikubwa uathiri matumizi ya ardhi na uwaathiri zaidi wanawake kuliko makundi mengine, hii ni kwa sababu wanawake ndio wanaotegemea ardhi zaidi kwa kilimo cha chakula ili waweze kutunza familia zao. Uzoefu unaonesha kuwa migogoro inapokithiri vijijini wanaume uhama familia zao na kwenda kwenye miji ya pembezoni au miji mikubwa kwa sababu ya kwenda kutafuta maisha zaidi na kuwaacha wake zao wakilelea familia wenyewe pasipo usaidizi wowote. Serikali iweke mikakati madhubuti ya kuipunguza au kuimaliza migogoro ya ardhi vijijini ili kuwawekea mazingira mazuri wakulima wadogo wadogo ikiwa ni pamoja na wanawake.

Kwa kuhitimisha, maadhimisho ya siku ya wanawake waishio vijijini yajikite katika kuibua changamoto zinazowakabili wanawake hao na wao wenyewe wawe ndio wahusika wakubwa katika kuzieleza na kuzijadili changamoto hizi na hata kutoa mapendekezo ya namna ambavyo wangetaka zitatuliwe. Yasiwe maadhimisho ambayo yanaadhimishwa na baadhi ya taasisi tu au kundi fulani la watu kama mradi tu bali kwa nia dhabiti ya kuhakikisha kuwa maisha ya wanawake wa vijijini yanaboresheka na kuwa na uhakika wa leo na kesho yao.

Na Cathbert Tomitho
HAKIARDHI